Search This Blog

Friday, September 19, 2014

Global Publishersyawaomba radhi ZittoKabwe na Diva

Kupitia gazeti la Amani la Septemba
11-17, 2014, kulichapishwa habari
ukurasa wa mbele iliyosomeka: “DIVA:
ZITTO NI MUME WANGU.” Ikikolezwa
na dondoo ‘Adai ni mke
anayetambulika kisheria’ na ‘Asema
hayuko tayari kuachana naye kirahisi,’.
Na sasa uongozi wa gazeti hilo
umekusudia kwa nia njema kutoa
ukweli juu ya habari hiyo.
Ufafanuzi huu unalenga kumaliza
mkanganyiko uliojitokeza hasa baada
ya kuwepo kwa madai kutoka kwa
mhusika ambaye ni Loveness Malinzi
(Diva) kuwa, hakuzungumza na gazeti
kile kilichoandikwa na kwamba
alikuwa anazushiwa; madai haya
aliyawasilisha chumba cha habari kwa
njia ya simu na sehemu kuyaweka
kwenye ukurasa wake wa kijamii wa
Instagram.
Kama hilo halitoshi, Diva alikana
kuzungumza na mwandishi wa habari
hiyo ambapo alisema mazungumzo
yao yalihusu mwaliko wa Kipindi cha
Global TV Online ambacho
kinarushwa na mtandao
unaoendeshwa na Kampuni ya Global
Publishers inayomiliki pia Gazeti la
Amani na si vinginevyo.
Malalamiko haya ya Diva yalikuja
muda mchache baada ya gazeti
kutoka likiwa na habari hiyo ambapo
jopo la wahariri wa Amani kabla ya
kuchapisha habari hiyo walijiaminisha
kuwa ni ya kweli kutokana na taarifa
pamoja na vielelezo vya rekodi ya
sauti ya mazungumzo
alivyoviwasilisha mwandishi kwenye
dawati kuthibitisha kuwa alifanya
mazungumzo na mhusika kuhusiana
na msingi wa habari nzima
iliyoandikwa.
Kama tulivyoeleza, baada ya habari
hiyo kutoka na kipande cha sauti
kuingizwa kwenye Tovuti ya Global
Publishers, ndipo yalipoibuka madai
hayo huku baadhi ya wasomaji
wakieleza kuwa ile siyo sauti ya Diva;
hapo ndipo uongozi wa gazeti
ulipoamua kufuatilia ukweli na kubaini
yafuatayo.
Pamoja na ukweli kuwa Mheshimiwa
Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma
Kaskazini) na Diva wana ukaribu,
mazungumzo kati ya mwandishi na
mwanadada huyo kuhusiana na kauli
yake ya: “Zitto ni Mume Wangu,”
hayakufanyika na kwamba mwandishi
alipika habari na kutengeneza sauti ya
Diva kwa lengo la kuwahadaa wahariri
kwa nia mbaya!
Kwa msingi huo sisi kama chombo
cha habari makini, kinachosimamia
weledi, kulinda na kuheshimu haki za
binadamu; tunachukuwa nafasi hii
kumuomba radhi Diva, Mheshimiwa
Zitto, sanjari na jamii kwa ujumla kwa
usumbufu wowote uliosababishwa na
habari hiyo. Aidha, uongozi unapenda
kuutangazia umma kuwa, hatua kali
za kinidhamu zimeshachukuliwa dhidi
ya mwandishi husika sambamba na
onyo kwa viongozi wote wa gazeti kwa
udhaifu uliojitokeza katika habari hiyo.
Tunaomba jamii ielewe kwamba
Global Publishers siku zote
inasimamia UKWELI na kamwe
hairuhusu kabisa habari za uongo
kuandikwa katika magazeti yake.
Jamii iendelee kutuamini na
kushirikiana nasi katika kusimamia
weledi wa uandishi wa habari.
Milango ya kukosolewa iko wazi, hivyo
kwa mwenye malalamiko yoyote juu
ya habari zetu, iwe ni uongo au
kutotendewa haki, asisite kuwasiliana
na viongozi kwa hatua zaidi. Ndimi,
Mhariri Kiongozi, Magazeti Pendwa.

0 comments:

Post a Comment