Search This Blog

Saturday, September 20, 2014

Azam Media Limited Wakabidhi Fungu La Pili Kwa Klabu Za Ligi Kuu TZ bara

Azam Media Limited Wakabidhi Fungu La Pili Kwa Klabu Za Ligi Kuu TZ baraKampuni ya Azam Media Limited, leo imekabidhi hundi ya Sh Milioni 423.5 kwa bodi ya ligi kuu ya vodacom Tanzania bara kwa ajili ya haki za matangazo ya Telesheni ya ligi hiyo.
Fedha zitagawiwa kwa klabu 14 za ligi kuu, Azam FC, Simba SC, Yanga SC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Ndanda FC, Polisi Morogoro, Coastal Union, Mgambo JKT, Stand United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mbeya City na Prisons kila kilabu ikipata Sh. Milioni 27.5, hiyo ikiwa ni awamu ya pili ya mgawo wa Sh. Milioni 110 za msimu.
Mtendaji mkuu wa Azam Media Limited, Rhys Torrington amesema sehemu ya fedha walizokabidhi hii leo ni awamu ya pili, na awamu mbili zilizobaki zitatolewa mzunguko wa pili wa ligi hiyo utakaoanza mwaka 2015.
“Nia ya Azam Media Limited kudhamini ligi kuu ni kutaka iwe na ushindani ambao utaleta mvuto na iwe nzuri zaidi miongoni mwa ligi za Afrika Mashariki,” Amesema bosi huyo wa Azam Media.
Amesema kwa sasa Azam Media Limited imetanua wigo wa huduma zake na inaonekana karibu nchi zote za ukanda wa Afrika mashariki na kati, hivyo ni imani yao ligi kuu itatangazika zaidi kimataifa.
Akizungumzia michezo ya ufunguzi ya ligi hiyo itakayochezwa mwishoni mwa juma hili, Torrington amesema wataonyesha michezo mitatu, ambayo ni kati ya mabingwa watetezi, Azam FC dhidi ya Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Simba SC dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mtendaji mkuu wa ligi kuu, Silas Mwakibinga amewashukuru Azam Media Limited kwa udhamini huo mzuri na kutekeleza vizuri Mkataba wao.
Mwakibinga pia ametoa wito kwa waamuzi wa ligi Kuu kutenda haki katika maamuzi yao ili timu bora zishinde.
“Na pia kwa kupata fedha hizi mapema, naamini sasa klabu hazitakuwa na visingizio wala kelele,”amesema Mtandaji mkuu wa TPL Board.
Amesema fedha hizo zilizotolewa leo, zinafanya kila klabu hadi sasa iwe imepata Sh. Milioni 55 baada ya kupewa fungu la sehemu ya kwanza mwezi Juni mwaka huu.
Azam Media Limited waliingia Mkataba wa haki za matangazo ya Televisheni ya ligi kuu mwaka jana na shirikisho la soka tanzania (TFF) kwa pamoja na bodi ya ligi, wakitoa Sh. Milioni 100 kwa kila klabu, wakati mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 10, na kufanya dau la Milioni 110.

0 comments:

Post a Comment