Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Yanga kuwasilisha
rasimu ya Katiba waliyoipitisha, kwa kuzingatia kuwa Muhtasari wa kikao
cha Mkutano Mkuu wao wa Juni 1 mwaka huu umeainisha baadhi ya
marekebisho waliyofanya kwa tulivyowaelekeza.
Yanga
wanatakiwa kuwasilisha rasimu hiyo kabla ya Oktoba 5 mwaka huu. Ikiwa
itakubaliwa na TFF, itapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo
ili waweze kufanya uchaguzi wa viongozi wao.(Martha Magessa)
TFF KUCHUNGUZA HUJUMA DHIDI YA STARS
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari zikielezea
tuhuma za hujuma kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi za kufuzu
mashindano ya AFCON.
TFF
pamoja na kutokuwa na uthibitisho wa tuhuma hizi nzito haliwezi
kuzikalia kimya. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania litateua jopo la
kuchunguza tuhuma hizi.
Wanafamilia
wa mpira wa miguu Tanzania (Members of TFF Family) watakaohitajika
kuhojiwa na jopo hilo kwa mujibu wa Ibara ya 37 ya Kanuni za Maadili za
TFF watalazimika kutoa ushirikiano. Atakayeshindwa kutoa ushirikiano
atachukuliwa hatua za kimaadili.
Pia wadau
wa mpira wa miguu ambao sio wanafamilia wa TFF, watakaoitwa na jopo
hili wanaombwa watoe ushirikiano kwa nia ya kujenga mpira wetu.
KATIBU COASTAL UNION KUPELEKWA MAADILI
Katibu
Mkuu wa Coastal Union, Kassim El Siagi atafikishwa kwenye Kamati ya
Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushinikiza
mkutano wa wanachama wa klabu hiyo ufanyike bila kuandaliwa na Kamati ya
Utendaji.
Pia El
Siagi alitumia vyombo vya habari kuishambulia TFF ambayo haikutambua
uamuzi wa mkutano huo ulioelezwa kumdumaza Makamu Mwenyekiti wa klabu
hiyo Steven Mnguto.
TFF ilimtuma Mkurugenzi wake Msaidizi wa Sheria na Uanachama kufanya uchunguzi wa mgogoro uliokuwa unaendelea katika klabu hiyo.
Baada ya
kupokea taarifa ya uchunguzi huo, TFF imebaini kuwa Mwenyekiti na Mweka
Hazina wa klabu hiyo walishajiuzulu, hivyo uitishwe uchaguzi haraka na
kujaza nafasi hizo na nyingine zilizo wazi.
Pia
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Coastal Union, Salim Amir na Albert
Peter wameonywa kwa kushiriki katika mkutano ambao wanajua haukuandaliwa
na Kamati ya Utendaji.
Vilevile
uchunguzi wa TFF umebaini kuwa ushiriki wa Salim Bawazir na Akida Machai
kwenye vikao vya Kamati ya Utendaji ya Coastal Union si halali kwa vile
wajumbe wa kamati hiyo wanachaguliwa na Mkutano Mkuu na si kuteuliwa na
Mwenyekiti.
Kwa vile
kutakuwa na uchaguzi wa kujaza nafasi ambazo zipo wazi, uchaguzi huo
utasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Coastal Union kwa kushirikiana na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga na
Coastal Union watafanya uhakiki wa reja ya wanachama.
BONIFACE WAMBURA
KNY KATIBU MKUU
- SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
0 comments:
Post a Comment